Pages

September 17, 2009

Mashindano ya Netiboli Kuanza Tarehe 28 Mwezi Huu.

Miaka minne ya kwanza ya uongozi wetu ilikuwa ni ya kujifunza. Wengi wetu tulioingia madarakani tulikuwa nje ya chama hiki, kwa hiyo tulihitaji kujifunza na kuona mambo yalikuwa yanaendeshwa vipi.Lakini baada ya miaka hiyo minne kupita, tulijua namna gani wenzetu waliokuwa wanaongoza chama hiki walivyokuwa wanafanya kazi zao, na wapi walipojikwaa na kushindwa kupiga hatua. Kisha tukaingia kwenye uchaguzi na baada ya uchaguzi sasa tumejipanga vyema kuhakikisha kuwa mchezo huu unapiga hatua zaidi na Tanzania kuingia kwenye ramani ya kimataifa",Hayo ni maneno ya Mwenyekiti wa chama cha mchezo wa mpira wa netiboli nchini, Anna Bayi alipokuwa anazungumzia maandalizi ya mashindano ya netiboli ya ya kimataifa yanayotarajia kuanza kutimua vumbi kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 3 mwaka huu. Soma zaidi....


Mashindano hayo ambayo yanatambuliwa na Shirikisho la kimataifa la mchezo huo (IFNA) yanatarajia kuzishirikisha nchi zaidi ya 10 ambazo ni Zambia, Kenya, Uganda, Malawi, Shelisheli, Botswana, Afrika Kusini, Lesotho, Namibia, Zambia, Rwanda na wenyeji Tanzania huku Rwanda wakijiandaa kuthibitisha.Jumla ya wanamichezo 108 kutoka katika nchi hizo wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo yatakayofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Timu ya Tanzania 'Taifa Queens' kwa muda mrefu iko kambini katika shule ya Filbert Bayi iliyopo kibaha mkoani Pwani ikijiandaa na mashindano hayo chini ya mwalimu wao kutoka New Zealand, aitwaye Cate Carpenter.Anna Bayi alisema kuwa katika miaka yao ya kujifunza, chama chake kimejifunza kuwa viongozi waliokuwepo madarakani hapo awali walikuwa wanauendesha mchezo huo kwa mazoea."Wengi tulikuwa tunajiuliza ni kwa nini CHANETA ilikuwa inashindwa kuuendeleza mchezo huu, lakini tulichojifunza ni kwamba, kufanya kazi kwa mazoezi lilikuwa tatizo sugu na kikwazo cha maendeleo ya mchezo huu," anasema Anna Bayi.Anasema viongozi wa awali walikuwa wanataka kufanya kila jambo wao wenyewe pasipo kushirikisha wadau wengine kutoka nje ya chama hicho ambao wangeweza kutoa mchango mkubwa zaidi."Sisi hilo tuliliona tukaona ni vyema tukawashirikisha wadau wangine kuuinua mchezo huu. Lakini hili lisingewezekana wakati tayari tulikuwa tumefutiwa uanachama wetu katika shirikisho la kimataifa la netiboli IFNA.
Kwa hiyo kazi ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha kuwa tunarudisha uanachama wetu," anasema Anna Bayi.Anasema mara baada ya kufanikiwa kurudisha uanachama, sasa kazi iliyopo ni kuitangaza Tanzania katika medani ya kimataifa, ikiwemo kuwafundisha wachezaji wao mbinu za kimataifa na kuandaa mashindano ya kimataifa."Mimi nilifanikiwa kwenda kushuhudia mashindano ya dunia yaliyofanyika nchini Uingereza. Lengo kubwa la kwenda kule ni kujaribu kuangalia nini wenzetu wanafanya pamoja na kuzungumza na wadau mbalimbali wa mchezo huu.
Naweza kusema kuwa safari yangu ilikuwa na mafanikio makubwa kwani niliweza kuona namna wenzetu walivyopiga hatua na kucheza kwa kutumia mbinu za kisasa. Pia niliweza kukutana na wadau mbalimbali ambao nilibadilishana nao mawazo na kunipa mbinu mbalimbali za kuendesha mchezo huu," anasema Mwenyekiti huyo wa CHANETA."Walinieleza kuwa ili tuweze kuingia kwenye medani ya kimataifa ni lazima tuwatengeneze wachezaji wetu wakiwa na umri mdogo, kwa hiyo ni lazima turudi mashuleni. Tulileta wataalamu toka nje ambao waliwafundisha wanafunzi na walimu wa shule 10 za mkoa wa Dar es Salaam kutoka Ilala, Temeke na Kinondoni.Programu hii kwa kweli imeanza kuzaa matunda kwani katika timu zinazoshiriki mashindano ya Mahanga Cup, wachezaji hao wameonekana kucheza kisasa zaidi na kuwa tofauti na wenzao. Tumeanza na shule hizi, lakini mpango wetu ni kufanya hivi kwa shule zote za Tanzania," anasema Anna Bayi.Bayi anasema kuwa sambamba na kampeni hiyo ya kukuza mchezo huo, pia chama chake kimejifunza kuwa kinahitaji kushirikisha wadau mbalimbali wa michezo nchini ili mchezo huo uweze kupiga hatua zaidi."Wenzetu waliopiga hatua zaidi wamefanikiwa kutokana na kuwashirikisha wadau mbalimbali, na sisi tumejifunza hilo kwani mchezo huu si wa CHANETA peke yake ni mchezo wa watanzania isipokuwa CHANETA ni wasimamizi tu,"Anasema kuwa katika kulifanyia kazi hilo, ndiyo maana wameunda kamati ya mashindano ambayo inawashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya chama hicho. Wadau wanaounda kamati hiyo ni Flora Kasambala, Rose Mkisi, Fatuma Miala, Edda Itende, Matilda Balama, Christina Malasusa, Sofia Upson, Sarah Kibonde na Mama Diamwale. "Unajua mashindano haya ni makubwa na yana sura ya kimataifa. Kuyaendesha ni gharama, kwa hiyo sisi kama CHANETA peke yetu tusingeweza.
Ndiyo maana tumeamua kuunda tume ambayo ina wataalamu wa nyanja mbalimbali," anasema Mwenyekiti huyo wa CHANETA."Tunaamini sisi kama viongozi wa CHANETA ni wazuri zaidi katika kuandaa mchezo, lakini kuna vitu vingi vinahitaji hadi mchezo kukamilika. Kwa hiyo tume yetu ina watu ambao wanaufahamu mkubwa na wameweza kutusaidia kwa kiasi kikubwa katika maandalizi," anasema Anna Bayi. Anasema anaamini mafanikio ya mashindano hayo yataweza kuipatia sifa Tanzania na kuiwezesha kuwa miongoni mwa nchi zinazoheshimika Afrika na duniani katika mchezo huo, na amewaomba wadau wengine ambao hawamo katika kamati hiyo kujitokeza na kukisaidia chama chake."Ndiyo kwanza tumerudi kwenye medani ya kimataifa. Kwa hiyo kwa kuandaa mashindano haya, lazima wadau wa mchezo huo duniani wataona kuwa tuna mipango madhubuti ya kuendeleza mchezo huu nchini kwetu. Lakini ili kufanikisha hili nawaomba wadao wote nchini wajitokeze watusaidie kwa hali na mali ikiwemo ushauri na mambo mengi," anasema.Bayi anasema kuwa mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo, washiriki wote watakwenda kutembelea mbuga za wanyama.

No comments:

Post a Comment