Welcome to pwaniraha blog please contribute by posting your comments on our blog, kindly note that abussive language is strictly not entertained. Thank you.
Welcome To Pwani Raha Blog; email us at "pwaniraha@gmail.com"

December 21, 2008

M'BILIA BELL












MWANAMUZIKI M’bilia Bell na Mkongo mwenzake, Felly Ipupa, juzi walifanya mambo yaliyowaacha hoi mashabiki wa muziki katika sherehe ya mwisho wa mwaka ya Embassy Club E iliyofanyika katika viwanja vya New World Cinema, Dar es Salaam. Kati ya wasanii hao, M’bilia ndiye aliyeonekana kuwagusa zaidi mashabiki hao ambao waliungwa na wateja wa sigara ya Embassy na marafiki zao kutokana na umahiri wake katika kuimba na kucheza.

Kikubwa zaidi kilichouacha hoi umati uliohudhuria sherehe hizo, ni jinsi mama huyo alivyokuwa akijituma jukwaani kwa kucheza nyimbo zake, huku akiwashirikisha mashabiki katika kuimba na kucheza. Na nyimbo zake zilizokuwa na mchanganyiko wa lugha ya Kiswahili, zilipokewa vizuri mno kwani mashabiki walionekana kuzielewa na hivyo kujumuika naye katika kuimba na kucheza. Baadhi ya nyimbo ambazo mwanamuziki huyo aliyetumbuiza kwa takribani muda wa saa 1.45, aliwapagawisha nazo mashabiki ni Nadina, Nairobi, Shauri Yako, Philemene, Mapenzi ya Pesa na nyinginezo.

Kama ilivyokuwa kwa M’bilia, Ipupa aliyepanda jukwaani kuanzia saa sita usiku, naye alijitahidi kuwasimamisha mashabiki kutoka kwenye viti vyao, japo kidogo alionekana kuwakera kutokana na kuchelewa kupanda jukwaani baada ya kuwatanguliza wanamuziki wake kabla ya kujitokeza takribani dakika 30 baadaye. Kwa ujumla sherehe ya juzi zilifana mno na kuthibitisha uhodari wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) kupitia chapa yake ya Embassy walivyo makini katika kuwapa wateja wao kile roho inapenda. Mbali na M’bilia na Ipupa, wasanii wa hapa nyumbani kama Banana Zorro na bendi yake ya B Band na kundi la Tanzania House of Talent (THT), nao walifanya mambo yalioufanya usiku huo kuwa wa kukumbukwa.

No comments: